
Mkuu wa Polisi Jamii Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Frimina Massao, amewataka wanawake wilayani humo kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili hususani ndoa za utotoni kwa kuibua na kutoa taarifa za matukio hayo badala ya kufanya siri na kukaa kimya.
ASP Massao amesema Jeshi la Polisi litaendelea na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto, huku wakitoa wito kwa jamii Wilayani humo kuhakikisha wanazuia vitendo hivyo kuanzia ngazi ya familia.
Ametoa wito kwa jamii kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya ukatili badala ya kuliachia jukumu hilo kwa Jeshi la Polisi pekee ama Maafisa wa Ustawi wa Jamii ambapo itasaidia kupunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo hivyo.
Kwa upande wake Bi.Flora Msilu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya amewataka Wanawake Wilayani humo kuepuka kwenda katika shughuli zao za uchumi hususani maeneo ya Stendi huku wakiwa na watoto wao kwani kwa kufanya hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kwa mmomonyoko wa maadili kwa watoto hao.
Aidha ametoa wito kwa Wanawake Wilayani humo kuwekeza katika elimu kwa watoto wao ili kuikomboa jamii kifikra na kuwa na kizazi bora huko baadaye.
Awali Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bi.Monica Mwailolo, ametaja sababu za uwepo wa matukio ya ukatili ambazo ni pamoja na mila na desturi na kukosekana kwa mgawanyo wa majukumu baina ya Wanaume na wanawake, kwani hali hiyo husababisha wanawake kushindwa kushiriki katika fursa mbalimbali kama zile za kiuchumi, uongozi ambapo huchochea zaidi ukandamizaji katika jamii.