Askari Polisi wanafunzi 3500 katika Chuo Cha Polisi (CCP), kilichopo mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. Wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kilelektroniki wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF Kidigitali).
Akizungumza kwenye zoezi hilo Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Michael Bujiba, amesema, PSSSF imefika Chuo Cha Polisi Moshi ili kuwasajili Askari Wanafunzi ambao wako katika hatua za mwisho za kuhitimu mafunzo yao.
Amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imeweka msukumo wa kutaka Taasisi za Umma ziboreshe utoaji wa huduma kwa kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia.
“Bodi na uongizi wa PSSSF uliliona hili mapema na kinachotupa umahiri hivi sasa ni uendeshaji wa huduma zetu Kidigitali, mifumo yetu yote ya usajili wa wanachama, shughuli za ulipaji mafao, malipo ya wastaafu lakini pia uwasilishaji wa madai mbalimbali unafanyika kupitia mtandao kwa maana ya PSSSF Kidigitali.” Amefafanua Bw. Bujiba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mafao ya Fidia, Makao Makuu ya Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Basil Pandisha, amesema mfumo huo ni mzuri na unarahisisha utoaji wa huduma.
“Utawafanya waweze kupata taarifa zao pindi watakapoanza kazi, hakuna haja tena ya kutumia makaratasi, mtandao unafanya taarifa zipatikane kwa urahisi zaidi wakati wote.” Amesisitiza.