
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ametangaza rasmi kuwa yuko tayari kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Odinga amezungumza hayo jijini Nairobi ambapo amesema amechukua uamuzi huo baada ya mashauriano mengi na marafiki zake kote barani afrika.
Odinga alikuwa ameandamana na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, ambaye amesema umewadia wakati wa uenyekiti wa AU kushikiliwa na kanda ya afrika mashariki.
Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki kutoka Chad ambaye muhula wake wa kuhudumu utakamilika mwezi Februari mwaka ujao baada ya kuhudumu kwenye wadhifa huo tangu mwaka wa 2017.
Nchini Kenya, uamuzi huo wa Raila Odinga, unachukuliwa kuwa ni njia ya kustaafu siasa za kenya, baada ya kuwania urais mara tano na kushindwa.
