Back to top

RAIS  AJIUZULU BAADA YA MWAKA MMOJA MADARAKANI.

21 March 2024
Share

Rais wa Vietnam Vo Van Thuong amewasilisha barua yake ya kujiuzulu siku ya Jumatano, baada ya mwaka mmoja tu madarakani.

Taarifa ya kujiuzulu kwake imetangazwa na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo ya kikomunisti, inayotangaza kuanzisha operesheni kubwa ya kupambana na rushwa.

Taarifa zinasema Rais Vo Van Thuong alikiuka "kanuni" ambazo hazijabainishwa, na alishindwa kuonesha mfano kama mkuu wa nchi.

Tangazo hilo la kustaajabisha la kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 53 linakuja wakati Vietnam ikikumbwa na msukosuko mkubwa wa kisiasa, na ikumbukwe kuwa  mtangulizi wake pia alitimuliwa mamlakani kama sehemu ya operesheni ya kupambana na ufisadi ambayo ilishuhudia mawaziri kadhaa wakifukuzwa kazi na viongozi wa makampuni ya serikali wakifikishwa mahakamani kwa ulaghai na ufisadi.