
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameahidi kupandisha mishahara ya wafanyakazi baada ya kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuimarisha uchumi na ajira kwa wananchi wengi wa Tanzania.
Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi duniani ambayo imefanyka mkoani Iringa Rais Magufuli amesema anawapenda na kujali maslahi ya wafanyakazi lakini anaona ni muhimu zaidi kuwekeza fedha kwenye miradi ya kujenga uchumi ili mishahara itakapopandishwa uwe mikubwa na yenye kukidhi mahitaji muhimu ya wafanyakazi.
Kuhusu wafanyakazi kuhamishwa vituo vya kazi bila kulipwa stahiki zao Rais ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wakurugenzi wanaokwenda kinyume na maagizo ya serikali yake.
Akisoma risala ya wafanyakzi Katibu mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA Dk. Yahaya Msigwa ameeleza kilio cha wafayakazi ikiwemo kodi kubwa kwenye mishahara na kupandishwa kwa kima cha chini cha mshahara.
Wakitoa salamu za Meimosi spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi vijana na watu wenye ulemavu mheshimiwa Jenista Mhagama wameahidi kuimarisha ushirikiano na wafanyakazi ikiwemo kuboresha mslahi na baadhi ya sheria ambazo ni kandamizi.
Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mwaka huu yamehanikizwa na kaulimbiu inayosema kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kulenge kuboresha mafao ya mfanyakazi