Back to top

Rais Magufuli atoa msamaha kwa wafungwa 3,319.

26 April 2018
Share

Katika kuadhimisha miaka 54 ya muungano wa Tanzania Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,319.

Taarifa iliyosainiwa na katibu mkuu wizara ya mambo ya ndani ya nchi meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira imesema kati ya wafungwa hao, 585 wataachiliwa huru na 2,734 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huo.

Msamaha huo wa Rais unahusu wafungwa wagonjwa wa ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wako hatua za mwisho waliothibitishwa na jopo la madaktari , wazee , wenye ulemavu, walioingia na mimba gerezani pamoja na wenye watoto.

Aidha, msamaha wa Rais hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua, waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani na waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama , waliofungwa kwa rushwa, majambazi, wabakaji, wahujumu uchumi, majangili na wafanyabiahsara ya viungo vya binadamu.