Rais Dkt. JOHN MAGUFULI amewataka watanzania kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Muungano ya mwaka huu isemayo Muungano Wetu ni wa Mfano Duniani Tuuenzi, Tuulinde, Tuimarishe na Kuudumisha kwa Maendeleo ya Taifa Letu.
Rais ametoa changamoto hiyo alipolihutubia taifa kutoka uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma katika maadhimisho ya miaka hamsini na minne ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amewataka Watanzania waulinde na kuudumisha muungano ambao amesema ni wa kuigwa duniani.
Ameyataja baadhi ya mafanikio ya muungano huo kuwa yamewawezesha Watanzania kudumu katika umoja, amani na kuheshimiwa na jamii ya kimataifa.
Amewapongeza waasisi wa Muungano Baba wa Taifa Mwalimu JULIUS KAMBARAGE NYERERE na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati ABEID AMMAN KARUME.
Aidha ameutangaza mji wa Dodoma kuwa jiji kuanzia leo na kuifanya Tanzania kuwa na majiji sita.
Majiji mengine ni Dar es salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza na Tanga.
Maadhimisho hayo yameshereheshwa pamoja na mambo mengine kwa gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Watanzania, maonesho ya majeshi ya ulinzi na usalama kuhusu ukakamavu wa kuilinda nchi, halaiki na burudani za ngoma mbalimbali.
Leo ni mapumziko Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dakta REGINALD MENGI pamoja na uongozi wa ITV/Radio One unawatakia kila la kheri katika maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.