
Rais wa Kenya, William Ruto, amesema gharama iliyotumika kukodi ndege wakati wa ziara yake ya siku nne nchini Marekani, ni ndogo zaidi kuliko angeondoka na ndege ya shirika la ndege la nchi hiyo (Kenya Airways).
.
Rais huyo aliondoka nchini Kenya Mei 19, 2024, kuelekea Marekani kwa kutumia ndege ya kukodi aina ya Boeing 737-700, inayodaiwa kumilikiwa na kampuni ya Royal Jet ya Dubai, ambapo imeelezwa kuwa kutoka Nairobi hadi Atlanta kwa kutumia ndege hiyo ya kifahari, kwa safari inayochukua takriban saa 18, gharama yake ni takriban Ksh. milioni 98/-, hivyo kwenda na kurudi inaweza kuwa zaidi ya Ksh. milioni 190/-.
.
Ruto ameeleza hayo baada ya watu wengi kuhoji juu ya gharama hiyo ambayo imeonekana kuwa kubwa, huku wengine wakimlaumu Rais huyo kwa kwenda kinyume na maelekezo yake kwa watumishi wengine wa umma ya kuwa waishi kulingana na uwezo wao.
.
“Wakenya wenzangu, nimeona wasiwasi wenu kuhusu usafiri niliotumia kwenda Marekani. Kama msimamizi anayewajibika wa rasilimali za umma na kulingana na azimio langu...la kuishi kulingana na uwezo wetu na kwamba ninafaa kuongoza...kufanya hivyo, gharama ilikuwa ndogo kuliko kusafiri kwa KQ(Kenya Airways)," ameeleza Ruto kupitia X.Com.
