
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kufungua Mkoa wa Katavi kwa kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Rais Dkt. Samia amesema hayo mkoani Katavi, wakati akihitimisha ziara yake Mkoani humo na kukagua mradi wa barabara ya Kibaoni - Sitalike (km 74) sehemu ya Kibaoni - Mlele (km 50) inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“Niwaahidi wana Katavi jicho la Serikali lipo katika Mkoa huu, Lengo ni kuufungua Mkoa wa Katavi kwa njia zote na kama mnavyojua Bandari ya Karema tumeshaimaliza na imeanza kazi na sasa tunaenda kujenga barabara inayounganisha Bandari hiyo ili kufikisha bidhaa na mazao katika Soko”, amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameeleza kuwa amesikia kilio cha kuchelewa kwa ujenzi barabara ya Kibaoni - Mlele (km 50) ambao ujenzi wake umefika asilimia 15 wakati mpango kazi ilitakiwa kufika asilimia 30 na kuahidi kuikamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuhakikisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wa Mpimbwe kuwa ujenzi wa barabara ya Kibaoni - Mlele utekelezaji wake utaaanza kwenda kwa kasi ile inayotakiwa baada ya kufanyia kazi changamoto zilizokuwa zinamkabili Mkandarasi huyo.