
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuna umuhimu wa kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuwasaidia wafungwa wanaomaliza vifungo vyao ili waweze kuanza maisha mapya baada ya kutoka magerezani.
Rais Samia amesema hatua hiyo itasaidia wafungwa waliopata mafunzo ya ujuzi gerezani kuanzisha shughuli za kujitegemea na hivyo kupunguza uwezekano wa kurejea tena kwenye vitendo vya uhalifu.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 09, 2026 wakati akihitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi Na. 28 pamoja na Uongozi Daraja la Pili Kozi Na. 48 yaliyofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam.
Rais Samia amesema tayari amekuwa akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Magereza pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu uwezekano wa kuanza sera ya kuwachangia wafungwa wanaomaliza vifungo vyao.
“Jeshi la Magereza lianzishe mfuko maalum kwa wale wafungwa wanaotoka na ujuzi mzuri kuanza kupatiwa chochote cha kwenda kuanzia kazi ili wafungwa wasiwe wanarudi tena kwenye magereza,” amesema Rais Samia.
Amesema pamoja na kutoa mafunzo kwa wafungwa, ni muhimu Serikali kuweka mfumo wa kufuatilia matokeo ya mafunzo hayo baada ya wafungwa kurejea katika jamii ili kupima mafanikio ya programu za urekebishaji.
Kwa mujibu wa Rais Samia, hatua zinazochukuliwa na Jeshi la Magereza katika kuimarisha mipango ya urekebishaji wa wafungwa zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuwa na taasisi imara zinazochochea amani, ustawi wa jamii na maendeleo jumuishi.
Aidha, amesisitiza watumishi wa Jeshi la Magereza kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, haki, usawa na maslahi ya taifa.
