Back to top

Rais Samia apokea ujumbe maalum wa Mhe. Rais Kenyatta.

10 April 2021
Share

Pamoja na kupokea ujumbe huo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia amefanya mazungumzo na Mhe. Balozi Amina kuhusiana na dhamira ya Tanzania na Kenya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali hususani kiuchumi na kijamii.

Mhe. Rais Samia amemhakikishia Mhe. Rais Kenyatta kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kuendeleza mambo mazuri yote yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kutatua changamoto kati ya Tanzania na Kenya kwa kuwa nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ndugu, majirani na marafiki wa kihistoria.

 

Amewataka Mawaziri na Wataalamu wa Tanzania na Kenya wanaounda Kamati ya Ushirikiano wa Pamoja (Joint Permanent Commission – JPC) ambao hawajakutana tangu mwaka 2016 kukutana mara moja ili kufanyia kazi masuala mbalimbali ya
kuimarisha uhusiano.

Mhe. Rais Kenyatta amemwalika Mhe. Rais Samia kufanya ziara rasmi nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano.

Amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Kenya ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania kwa kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Amina ameongozana na Balozi wa Kenya hapa nchini, Mhe. Dan Kazungu.