Back to top

RAIS TSHISEKEDI AKUBALI MAZUNGUMZO NA KAGAME

28 February 2024
Share

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi amesema yuko tayari kuzungumza na mwenzie wa Rwanda Paul Kagame ili kukomesha machafuko mashariki mwa Congo.

Kufuatia mkutano wa ana kwa ana wa masaa matatu mjini Luanda, Angola, Rais Felix Tshisekedi na mwenyeji wake Joao Lourenco hawakutoa kauli yoyote mbele ya waandishi habari.

Lakini waziri wa mambo ya nje wa Angola, Tete Antonio amesema Tshisekedi amekubali kuzungumza na mwenzake Paul Kagame wa Rwanda.

Hatua ya Tshisekedi kukubali mazungumzo na Kagame imekuja miezi mitatu baada ya kiongozi huyo kuapa kwamba hawezi tena kukutana na jirani yake huyo hadi mbele ya Mungu. 

Hata hivyo, Ikulu ya Kongo tayari imetoa masharti kabla ya mkutano wowote baina ya Tshisekedi na Kagame ikiwemo kuondolewa mara moja kwa wanajeshi wa Rwanda katika eneo la Kongo.