Back to top

Rais wa Tanzania atoa msamaha kwa wafungwa wapatao Elfu 5 na 533.

09 December 2019
Share

Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa wapatao Elfu 5 na 533 nchi nzima leo Disemba 9, 2019, ambapo wafungwa hao wataanza kuachiwa kuanzia kesho Disemba 10, 2019, ambapo amesema msamaha huo unawalenga wafungwa waliofungwa Kati ya siku moja na mwaka mmoja.

Wafungwa wengine watakao husika na msamaha huo amesema ni wafungwa waliofungwa miaka 30, miaka 20, miaka 10 na miaka 5, lakini tayari wametumikia sehemu yao kubwa ya vifungo vyao na kubakiza kipindi kisichozidi mwaka mmoja watahusika na msamaha huo.

Rais Magufuli ametoa msamaha katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru na miaka 57 ya Jamhuri ya Tanganyika, katika uwanja wa CCM  Kirumba jijini Mwanza, huku akisema amelazimika kutoa msamaha huo kwa siku ya leo baada ya kutembelea magereza na kushuhudia  mlundikano wa wafungwa ambapo mpaka leo kuna Wafungwa 17,547 na Mahabusu 18,256 nakusema idadi hiyo ni kubwa kwani baadhi wamefungwa kwa makosa madogo madogo tu.

Amesema ni wazi watu watamshangaa kwa kutoa msamaha kwa idadi kubwa ya wafungwa wapatao Elfu 5 na 533 nchi nzima lakini imebidi kama mwanadamu na hali aliyojionea katika gereza la Butimba ilimhuzunisha sana, kumsikitisha kwani hali ilikuwa mbaya sana hivyo kwakutambua kwamba hakuna binadamu aliyemkamilifu na kwamba sisi wote tunamkosea mungu naye amekuwa akitoa msamaha, na kwakutambua dini zote zinafundisha kusamehe, hivyo amewasamehe wafungwa hao.

Pia Rais Dkt.John Magufuli ameeleza mikoa inayoongoza kwa wafungwa wengi na ambao katika msamaha wa leo ameguswa na kutoa msamaha ni pamoja na Kagera ambao unaidadi ya wafungwa 713.

"Mkoa unaoongoza kwa wafungwa wengi watakao samehewa ni Mkoa wa Kagera wako 713, Mkoa wa Dodoma 385, Morogoro wapo 365, Dar es Salaam 293, Mara 260, Mbeya 259, Kigoma 252, Tanga 245, Geita 230, Rukwa 214, Arusha 208, Manyara 207, Tabora 207, Mwanza 190, Ruvuma 181, Singida 139, Simiyu 136, Lindi 129, Pwani 128, Iringa 110, Songwe 96, Katavi 74, Shinyanga 74 na Njombe wafungwa 70"-Rais Magufuli 
 
Jamhuri ya Tanganyika ni mshirika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopatikana baada ya kuungana na Zanzibar, Aprili 26 mwaka 1964.

Aidha licha kutoa msamaha kwa wafungwa Rais alipata pia wasaha wa kuyaelezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho cha Uhuru kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, kuimarisha huduma za afya, elimu na hata idadi ya watu.

Amesema jukumu la serikali ya awamu ya tano anayoiongoza ni kuyalinda mafanikio hayo yaliyoanzishwa na awamu zilizotangulia, na kuwapongeza viongozi waliomtangulia kwa kuyaanzisha mafanikio hayo pamoja na wananchi kwa mshikamano wao.

Kwakati wa maadhimisho hayo Rais ameshuhudia manonesho mbalimbali yakiwemo ya kijeshi na ngoma za asili.