Back to top

RC Chalamila kuwachukulia hatua watumishi wahujumu miradi ya maendeleo

09 June 2021
Share

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Albert Chalamila amesema hatasita kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watumishi wa umma watakaobainika kuhujumu miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na wale wanaosababisha migogoro kwa wananchi kwa maslahi yao.
 
Chalamila amesema serikali haitawafumbia macho watumishi wa umma wanaohujumu miradi ya maendeleo pamoja na kusababisha kero mbalimbali kwa wananchi.
 
Mkuu huyo wa mkoa wa mwanza, ambaye alikuwa akizungumzia ziara ya siku tatu ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani humo, amesema zaidi ya wakazi 60,000 wa mji wa Misungwi na maeneo jirani wanatarajia kunufaika na mradi wa maji uliopo katika kijiji cha Nyahiti uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 13.7.
 
Miradi mingine ya kimkakati ambayo Rais Samia ataifungua na kuiwekea mawe ya msingi katika mkoa wa Mwanza ni pamoja mtambo wa uchenjuaji dhahabu Mwanza uliopo Ilemela, ufunguzi wa jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kanda ya Mwanza, uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa 'SGR' eneo la Fella kati Mwanza hadi Isaka, pamoja na kutembelea na kukagua ujenzi wa daraja la kigongo – Busisi, maarufu kama daraja la JPM.
 
Ziara ya Rais Samia itakamilika juni 15 kwa kuongea na vijana wa mkoa wa Mwanza wa makundi mbalimbali ya kijamii.