Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa [TAKUKURU] wilayani Chamwino kumkamata na kumuhoji Afisa Manunuzi wa wilaya hiyo Ebby Mwakajila kwa tuhuma za upotevu wa shilingi Milioni 13 za ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mpwayungu na kumuagiza Mkurugenzi kumuondoa mara moja afisa huyo kwenye miradi yote ya maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa anatoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya klichopata fedha za serikali shilingi Milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa maabara wodi ya kinamama na watoto chumba cha upasuaji pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti.
Awali akisoma taarifa kwa mkuu huyo wa mkoa mjumbe wa kamati ya ujenzi Amani Mazengo amesema afisa huyo wa manunuzi amekuwa akiwalazimisha kununua vifaa kwa bei ya juu sehemu ambayo ana maslahi nayo bila kuzingatia thamani ya fedha.
kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk James Kihologwe ameeleza namna utaratibu wa mgao wa fedha za ukarabati wa vituo vya afya huku mpango wa matumizi yake huwashirikisha wananachi ambao huainisha changamoto zinazowakabili katika eneo lao.