Back to top

RC Mwanza avunja mkataba wa ujenzi kituo cha afya Nyamiswi Buchosa.

06 April 2018
Share

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ameuvunja mkataba wa ujenzi wa kituo cha afya Nyamiswi kilichopo kwenye kisiwa cha Kome katika halmashauri ya wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza, huku akiiagiza taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa( TAKUKURU) wilayani humo kupitia upya matumizi na manunuzi ya vifaa vya mradi huo uliotengewa Shilingi Milioni 400, baada ya kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo.

Mradi huu wa uboreshaji wa miundombinu ya Afya, unaojengwa na mafundi wa kienyeji ujenzi wake unaonekana kuendelea katika hali ya kusuasua licha ya kutakiwa kukamilika mei 15 mwaka huu.

Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Buchosa Dkt. Chacha Ernest, amesema hadi sasa zaidi ya Shilingi Milioni 218 zimetumika.

Mhandisi wa halmashauri ya wilaya hiyo Chagu Maliatabu Ngh'oma ameshindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusiana na mradi huo.

Emmanuel Kipole ni mkuu wa wilaya ya Sengerema amempa siku 7 fundi Herbet Mhalila anayetekeza mradi huo kupitia force akaunti kulingana na maelekezo ya serikali kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa maboma hayo kabla ya muda wa mkataba kuisha.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Buchosa Joseph Kanyumi, naye amejikuta hatiani baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na kliniki ya wazazi na watoto saa chache kabla ya mkuu wa mkoa huo kuanza ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya nyamiswi.