
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw.Said Mtanda amelipiga marufuku kundi linalojiita 'Kamchape' linalohusishwa na ramli chonganishi ya kuwaibua wachawi katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza akisema huo ni uchonganishi na kwamba Serikali haiwezi kuruhusu jambo hilo.
Mtanda amepiga marufuku vitendo vya kishirikina wilayani Ukerewe akiwa katika ziara ya ukaguzi wa Hospitali ya Mkoa yenye hadhi ya rufaa inayojengwa wilayani humo, Mtanda ametoa tamko hilo akieleza kuwa hakuna mtu atakayekubalika kufanya shughuli za ramli chonganishi ndani ya Mkoa wa Mwanza, akisisitiza kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kuendesha vitendo vya aina hiyo, sio tu Ukerewe bali mkoa mzima.
Aidha, Mtanda amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa hatua kali za kisheria zinachukuliwa kwa wale watakaobainika kuendelea na shughuli hizo.
Pia amekumbusha kuwa vitendo vya kishirikina vinavyohusishwa na kundi la 'Kamchape' vinavuruga amani na utulivu wa jamii, na kwamba serikali haitavumilia wala kupuuza vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama wa wananchi.
