Back to top

RC Songwe atembeza kichapo kwa wanafunzi waliochoma shule.

17 July 2020
Share

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela mapema leo amewachapa viboko wanafunzi watano waliohusika katika tukio la kuchoma moto shule ya sekondari ya Wavulana ya Oswe na kusababisha hasara ya Zaidi ya shilingi milioni 26.

Brig.Jen. Mwangela amefikia hatua hiyo mara baada ya kamati aliyoiunda ya kuchunguza chanzo cha ajali ya moto uliotokea shuleni hapo Julai 3 mwaka huu kubaini kuwa wanafunzi wawili Naftari Nganga na Collin Kisinga ndio waliochoma mabweni ya shule hiyo huku wenzao watatu wakiwa na taarifa za mipango hiyo  na hawakuripoti.

Amesema wanafunzi hao  walianza mpango wa kuchoma moto mabweni mnamo Juni 28 kwa kununua vifaa vya kuchomea, ilipofika Julai 2 walijaribu kuchoma bweni lakini halikuwaka, Julai 3 walichoma bweni likawaka na kusababisha hasara hiyo na Julai 6 walifanya jaribio lingine tena la kuchoma moto ghala la chakula lakini halikuwaka moto. 

Brig. Jen. Mwangela ametoa miezi mitatu kwa wazazi wa Naftari na Collin kila mmoja alipe shilingi milioni 7,300,000/= Mmiliki wa Shule pia alibainika kuwa na uzembe wa kuweka vifaa vya kuzimia moto hiyo alipie shilingi milioni 7,300,000/= huku mwalimu wa zamu siku ya tukio, mlinzi na Patroni nao wakitakiwa kulipa shilingi milioni 4 ili kufidia hasara iliyotokana na ajali hiyo ya moto.