Back to top

Ridhiwani Kikwete:Watendaji sekta ya ardhi tendeni haki.

14 May 2022
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanatoa haki wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.

Naibu Waziri Kikwete alieleza hayo alipokutana na watumishi wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Mbeya ambapo alioneshwa  kutoridhishwa na utendaji kazi wa baadhi ya watumishi wasiowaadilifu. 

Pia amesema baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi wamekuwa miungu watu kwenye maeneo yao kuliko hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ardhi yote iko chini ya mamlaka yake na kubainisha kuwa, mwananchi anaweza kwenda ofisi ya ardhi kwa ajili ya kumilikishwa ardhi lakini adha anayoipata wakati wa kuomba kupata uhalali wa kumiliki ardhi yake basi maafisa ardhi wamekuwa wakijizungusha bila kumsaidia.

Amebainisha kuwa utoaji haki uko katika sura tofauti kuanzia zoezi la utoaji hati, upatikanaji haki katika mabaraza ya ardhi na nyumba sambamba na utoaji taarifa na uwezeshaji wananchi katika ardhi au rasilimali ardhi.


"Kama kuna mtumishi anadhani kuna suala la kula kula ovyo kwenye Wizara hii ya ardhi basi siyo kwa nyakati hizi, ndugu zangu watendaji wenzangu naomba tuwe waadilifu katika kutenda haki kwa wananchi". Ridhiwani Kikwete.

Sambamba na hilo aliwataka Maafisa Mipango miji wa Mkoa wa Mbeya kuwa na mipango bora ya mipango miji ili jiji Mbeya lisiendelea kuwa jiji la makazi holela.