Back to top

RUKWA WAUNGA MKONO ZIWA TANGANYIKA KUPUMZISHWA

04 April 2024
Share

Wananchi Mkoa wa Rukwa wameunga mkono suala la upumzishwaji wa shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Abdallah Ulega.

Akizungumza wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa upumzishwaji wa shughuli za uvuvi wa ziwa Tanganyiaka, Wilayani Kalambo, Mkuu wa wilaya ya Kalambo akiwa kwenye  kikao hicho kilicho jumuisha madiwani, watendaji wa Kata na Vijiji, Mhe.Lazaro Komba, ameipongeza Serikali kwa uamuzi huo na kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na viongozi wa Kalambo, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za kulipumzisha Ziwa Tanganyika.

Mhe.Komba, amesisitiza kuwa ni vyema kupisha shughuliza za upumzishaji wa ziwa Tanganyika ,ili samaki waongezeke kwa wingi, baada ya shughuli za uvuvi kuendelea watu wakienda kuvua hao samaki wavue samaki wenye sifa za kwenda sokoni.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Kalambo, Bwana Daudi Schome, akiongea kwa niaba ya wananchi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ameeleza kuwa kusudio hilo limepokelewa vyema na wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo. 

Mheshimiwa Schome, amesema kuwa wananchi wameanza kuchukua hatua mbadala za kupata samaki kwa kuwakausha ili kuwatunza kwa matumizi ya kipindi chote ambacho ziwa litakuwa limepumzishwa. Pamoja na njia hiyo wananchi wamejiandaa kuendelea na shughuli za uvuvi katika mito, mabwawa ya kufugia samaki na maziwa mengine yaliyopo Mkoani Rukwa.

Vilevile, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uvuvi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya Uvuvi, Bi. Emelda Adamu amesema wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuchukua hatua kipindi ambacho ziwa Tanganyika litakuwa limepumzishwa.

Bi.Emelda ameongezea kuwa upumzishwaji wa ziwa Tanganyika utaenda sambamba na na tathimini mbalimbali za kibaiolojia, wingi na mtawanyiko wa samaki  na athari za kiuchumi na kijamii. Na zoezi la upumzishaji ziwa Tanganyika litakuwa kwa miezi mitatu kwa kila mwaka, ndani ya miaka mitatu.