Back to top

Sababu za ATCL kushikiliwa Afrika Kusini, Waziri Kamwelwe abainisha.

24 August 2019
Share

Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.Isack Kamwelwe ametolea ufafanuzi juu ya ndege ya Tanzania (ATCL) kushikiliwa na Mahakama kuu nchini Afrika Kusini huku akisema kuwa kutokana na hali hiyo wamesitisha safari nyingine za ndege za Tanzania kwenda nchini humo hadi watakapo jua sababu ya kukamatwa kwa ndege hiyo ya Tanzania, ambapo kwa sasa suala hilo linashughulikiwa na Mwanasheria mkuu wa serikali.

Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.Isack Kamwelwe.

Akizungumza na ITV kwa njia ya Simu Waziri Kamwelwe amekiri kuwa ndege aina ya Airbus 220-300 ya Shirika la ndege la Tanzania imezuliwa kuruka na kusafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo mjini Johannesburg, Afrika Kusini, hadi Dar es Salaam kuanzia jana Ijumaa.

Amesema Wizara yake imepokea taarifa kuwa ndege hiyo ilizuiwa kufuatia amri iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Gauteng mjini Johannesburg na mpaka sasa ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali inafuatilia jambo hilo.

Waziri Kamwele ameongeza kuwa mpaka sasa haikufahamika mara moja ni kwa nini ndege hiyo ilikamatwa na sababu za kufanya ikamatwe huku abiria waliokuwa wamepanda ndege hiyo kutafutiwa ndege nyingine ili waendelee za safari yao.