
Rais Samia Suluhu, Hassan ameridhia wananchi wa kitongoji cha Ikanka, Kijiji cha Itumba ,Wilaya ya Ileje, kuendelea kuishi sehemu ya eneo la hifadhi ya msitu wa Ileje Range, mkoani Songwe.
Uamuzi huo unakifanya kitongoji cha Nkanka sasa kitambuliwe ndani ya hifadhi ya msitu wa Ileje Range ,kutokana na idadi ya kaya 105 zenye makazi zilizopo ndani ya eneo.
Uamuzi huo pia umegusia mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi za msitu wa Mugombezi ,uliopo Kijiji cha Nyimbili ,katika kata ya Mlowo, Ilengo Mbozi mkoani Songwe.
Uamuzi wa Rais Samia umetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mh. Dkt Angeline Mabula, na kueleza kwamba, sehemu ya eneo la hifadhi, ekari 278 zitamegwa na kubaki kwa wananchi kutoka ekari 414 kwa kuwa eneo hilo limeendelezwa kwa shughuli za kilimo, makazi na kuwekwa huduma za kijamii kama uwanja wa mpira na Pump ya maji.
Waziri Mabula amewatahadharisha wananchi walioruhusiwa kuendelea eneo hilo kutojaribu kuongeza maeneo wanayoishi huku akieleleza kuwa, mara baada ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kukamilika maeneo yote ya hifadhi yanatakiwa kulindwa.
Aidha, Dkt Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikanka, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ameagiza Shughuli za kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji nazo zisitishwe ili kunusuru vyanzo vya maji ndani ya hifadhi.