
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Mhe. Samira Amour Khalfan, ameutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadhan pamoja na kipindi cha Kwaresma kuwatembelea watoto na wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo katika vituo vya kulelea na shule zenye wanafunzi wenye uhitaji maalum katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kagera.
Samira ameanza ziara hiyo, Februari 22, 2026 katika Wilaya ya Muleba kwa kutembelea Shule ya Msingi Kaigara yenye watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum.

Wakati huo huo, Katibu wa Mbunge, Edina Makoye, amewatembelea watoto wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Kashuro, vyote vikiwa vipo Muleba mkoani Kagera.
Katika maeneo hayo waliyoyafikia, Mbunge Samira amekabidhi mahitaji muhimu ikiwemo mchele, sukari, mafuta ya kupikia, unga wa ugali, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kujipaka pamoja na vinywaji kama juisi na biskuti.
Samira ameeleza kuwa dhamira yake ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuwaletea tabasamu wananchi, akisisitiza kuwa watoto na wanafunzi hao ni kundi linalohitaji kuoneshewa upendo, kuthaminiwa na kupewa furaha pamoja na matumaini.

Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kaigara, Samira amewatia moyo kusoma kwa bidii na kujituma, akieleza kuwa wao ni Taifa la kesho linalotegemewa.
Aidha, amewapongeza walimu na walezi wanaoendelea na jukumu la kuwalea na kuwahudumia watoto hao wenye mahitaji maalum, huku akibainisha kuwa utaratibu wa kuwafikia utakuwa endelevu katika vituo vyote vya Mkoa wa Kagera.
