Back to top

SAUDI ARABIA KUWEKEZA SEKTA YA MIFUGO NCHINI

17 March 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mazingira, Maji na Kilimo wa Saudi Arabia, Mhandisi AbdulRahman Bin Abdulmohsen Alfadley, ili kuona ni namna gani nchi hiyo ya Saudi Arabia inawekeza katika fursa zilizopo kwenye Sekta ya Mifugo hapa nchini.

Wakati Waziri Ulega akimkaribisha Waziri huyo wa Saudi Arabia, amesema kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kwenye Sekta ya Mifugo, hivyo anatamani kuona Saudi Arabia inafanya uwekezaji mkubwa katika eneo la malisho ya mifugo, biashara ya Nyama na ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba.

Aidha, Mhe. Ulega amemuhakikishia Waziri huyo kuwa hata kama wanataka kufanya biashara ya Mifugo hai, Serikali kupitia Wizara itahakikisha inaweka mazingira wezeshi biashara hiyo iweze kufanyika ikiwemo kuwawezesha kuweka karantini nzuri kwa ajili ya Mifugo.

Ulega amemueleza kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nia yake ni kuhakikisha sekta ya mifugo inaimarika kibiashara ili mchango wake kwa Taifa unakuwa mkubwa zaidi hivyo wanakaribisha uwekezaji ili kukuza uzalishaji katika Sekta hiyo.  

"Kwenye sekta ya mifugo tunahitaji uwekezaji mkubwa kwa sababu tuna rasilimali nyingi ikiwemo Maji, Ardhi na Mifugo, hivyo, tunatamani kuona katika makubaliano tutakayoyafanya, hayo mambo matatu yanajumuishwa katika mkataba wa makubaliano" Amesema Waziri Ulega

Kwa upande wake, Waziri wa Mazingira, Maji na Kilimo wa Saudi Arabia, Mhandisi AbdulRahman Bin Abdulmohsen Alfadley, Amesema kuwa wangependa kwa kuanzia wawekeze katika eneo la malisho ya mifugo aina ya alfalfa na biashara ya Nyama kutoka Tanzania kwenda Saudi Arabia.

Mawaziri hao kwa pamoja wamekubaliana kuanza mchakato wa kuandaliwa mkataba wa makubaliano ambao utaainisha maeneo ambayo nchi ya Saudi Arabia watafanya uwekezaji hapa nchini.