Back to top

Sekta binafsi injini sekta ya mifugo.

06 January 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema sekta ya binafsi ndio msingi wa maendeleo ya sekta ya mifugo kwa sababu ushiriki wao umekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza sekta hiyo nchini. Waziri Ndaki ameeleza hayo alipotembelea kiwanda cha kuchakata maziwa cha ASAS kilichopo mkoani Iringa.

Akiwa kiwandani hapo ameeleza kuwa wawekezaji katika sekta ya mifugo kama kina ASAS wakiwa wengi ni jambo zuri kwa maendeleo ya uchumi wa nchi kwa sababu uzalishaji wanaoufanya unachangia ukuaji wa pato la Taifa na kujenga afya za Wananchi.

"Serikali tunajivunia kuwa na wazalishaji wa maziwa kama nyinyi, na sisi kama serikali tunawaahidi tuko pamoja nanyi ili kuweza kuinua uchumi wa nchi yetu", amesema Mhe. Ndaki

Ameongeza kuwa serikali iko macho kuangalia changamoto zinazowakabili wawekezaji hao na kuhakikisha zinapungua makali yake ili waweze kufanya kazi kwenye mazingira mazuri pamoja na  wadau wao.

Kuhusu unywaji mdogo wa maziwa nchini, Waziri Ndaki amesema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wameshaanza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhamasisha unywaji wa maziwa ili wanachi wajenge utamaduni wa kunywa maziwa kwa wingi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji, Kiwanda cha ASAS, Fuad Jaffer aliipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka tozo  kwa bidhaa zinazotoka nje jambo ambalo limewapa wawekezaji wa ndani moyo wa kuendelea kuwekeza zaidi katika Sekta ya mifugo.

Aidha, ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikisha vyuo vinavyozalisha Maafisa Ugani na taasisi za utafiti kuwa wabia na wachakataji wa maziwa nchini ili kuzielewa changamoto ambazo wanazipata kwa wafugaji na kwa kufanya hivyo wataalam hao wanaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kuelimisha wafugaji kuzalisha maziwa yenye ubora.