Back to top

SEKTA YA MIFUGO KUGAWA MADUME BORA YA NG'OMBE

25 November 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema ugawaji wa madume ya bora ya ng’ombe ni utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo.

Waziri Ndaki ameeleza hayo wilayani Chamwino Mkoani Dodoma wakati alipokuwa anagawa madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran ambapo kila mmoja ana uwezo wa kupanda majike 25 kwa mwaka, kwa vikundi vya wafugaji kwa lengo la kwenda kuboresha mifugo yao ambayo mingi ni ya asili.

Ng’ombe wa asili huzalisha nyama kilo 80 -120 kwa ng’ombe wakati baada ya kuboreshwa kwa kosaafu mfugaji anaweza kupata kilo 150 – 200 kwa ng’ombe. Lakini pia kwenye upande wa maziwa ng’ombe hawa walioboreshwa kosaafu huwa na uwezo wa kutoa kati ya lita 5 – 10 za maziwa na hivyo kumfanya mfugaji apate tija zaidi tofauti na mfugaji wa ng’ombe wa asili.

Wafugaji wametakiwa kuyatunza madume hayo kwa kufuata taratibu zote wanazoelekezwa na wataalam wa mifugo.  Lakini pia Waziri Ndaki amevitaka vikundi ambavyo vimepatiwa madume hayo kuyatumia kwa kushirikiana na wafugaji wengine ili kuhakikisha tija inapatikana kwa wafugaji ndani ya Wilaya ya Chamwino.

Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema Wizara inaendelea kutekeleza mpango wa mabadiliko wa sekta hiyo ambapo licha ya kazi ya uboreshaji wa kosaafu inayoendelea, wafugaji wanaendelea kupatiwa elimu kuhusu malisho ya mifugo.

Wizara inaendelea kuanzisha mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwa lengo la kutoa elimu ya kilimo cha malisho na namna ya kuyatunza malisho hayo pamoja na nyanda za malisho ili malisho hayo yaweze kuwasaidia wakati wa kiangazi kikali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya amesema kuwa uongozi wa Wilaya utakwenda kusimamia utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo kwa kuhakikisha madume hayo yaliyogawiwa kwenye vikundi yanatunzwa na kutumika ili kuboresha kosaafu.

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Sekta ya Mifugo, Bw. Stephen Michael amesema kuwa takribani asilimia 97 ya ng’ombe waliopo nchini ni wa asili hivyo katika kutekeleza mpango wa mabadiliko wa sekta, Wizara imepanga kununua mitamba 1,160,000 ambayo itapelekwa kwenye mashamba ya serikali. Hivyo kutokana na uzalishaji wake wafugaji wataweza kupata ng’ombe bora hapa nchini badala ya kutegemea kuagiza kutoka nje.

Aidha, Wizara inaendelea na zoezi la uhimilishaji mifugo ambapo tayari imeshapanga kuhimilisha takribani ng’ombe 373,000 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye maeneo ambayo hawatapata madume hayo.

Mwakilishi wa taasisi ya PASS Trust, Langelika Kalebi amesema kuwa taasisi hiyo ni mwezeshaji ikichochea maendeleo kwenye kilimo (mifugo, uvuvi, mazao, na mazao ya porini). Taasisi hiyo ipo nchi nzima ikichochea maendeleo kwenye upatikanaji wa mitaji na elimu, hivyo wanaongezea dhamana katika kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa mtu mmoja, vikundi, vyama vya ushirika.

Naye mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Chamwino, Bw. John Kochocho ameishukuru serikali kupitia Sekta ya Mifugo kwa kuwapelekea wafugaji madume hayo ya ng’ombe yatakayokwenda kuboresha kosaafu na hivyo kuwafanya wazalishe kwa tija na kibiashara.

Serikali ya awamu ya sita ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kununua jumla ya madume bora ya ng’ombe wa nyama 366 aina ya Boran kama sehemu ya jitihada za kuendelea kuboresha tija ya ng’ombe tulionao nchini.