Back to top

Sendeka aiagiza TAKUKURU kumkamata mhandisi wa maji Makete kwa kugushi

16 July 2019
Share


Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe.Christopher Ole Sendeka ameamuru Kaimu Mhandisi wa Maji wilaya ya Makete mkoani Njombe, Daniel Sanga kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi mkoani Njombe, kwa hatua za kisheria, mara baada ya kutuhumiwa kutenda kosa la kughushi nyaraka za halmashauri hiyo kwa lengo la kutoa upendeleo kwa mmoja wa waombaji wa zabuni ya kujenga mradi wa maji wilayani humo.

Mhe.Sendeka licha ya kuchukua hatua hiyo pia ameionya kamati ya fedha na mipango ya halmashauri hiyo, kwamba haitabaki salama kutokana na kushindwa kuzingatia na kusimamia sheria za manunuzi na kulazimika ofisi ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali(CAG), kuibua hoja zinazopelekea harufu ya ufisadi wa fedha za umma.

Aidha katika kikao hicho cha baraza maalum la madiwani la kupitia hoja za mkaguzi mkuu wa serikali (CAG) katika halmashauri ya wilaya ya Makete kimefanyika wakati halmashauri hiyo ikiwa imepata hati yenye mashaka, jambo ambalo mkuu wa wilaya hiyo Veronika Kessy amelazimika kuanisha moja ya sababu zilizopelekea kuapata hati hiyo,na kwamba watumishi wa umma watakaobainika kufanya ndivyo sivyo kwenye fedha za umma hatua kali zitachukuliwa.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa halmashauri ya Makete imepata hati ya mashaka kwa mwaka wa fedha 2018/2019 hii ni kutokana na watumishi wa halmashauri hiyo wa idara mbalimbali kufanya kazi bila ushirikiano, jambo ambalo baadhi ya watumishi hao wanaotuhumiwa kwa kughushi nyaraka wakalazimika kutoa  utetezi mbele ya mkuu wa mkoa wa Njombe Mhe.Christopher Ole Sendeka, ambao haukuwa msaada kwao.

Katika kikao hicho mara kadhaa kililazimika kusimama kwa masaa  kadhaa hii ni kutokana na kile kilichodaiwa baadhi ya watumishi kukosa weledi katika utendaji wa kazi zao, kauli ambayo inaungwa mkono na katibu tawala wa mkoa wa Njombe, Kichere.