Back to top

SERIKALI HAIKUSITISHA TAA ZA SOLA KWA WAVUVI

31 December 2022
Share

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekanusha taarifa iliyosambaa hivi karibuni ya kusitishwa kwa matumizi ya Taa za Sola zinazotumia betri za pikipiki katika Uvuvi wa Dagaa kwenye Ziwa Viktoria kuanzia Januari Mosi 2023 huku ikiwataka wavuvi hao kuendelea na shughuli zao kwa kutumia zana na njia rafiki zinazolinda rasilimali za Uvuvi.

Kanusho la Serikali limetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Magese Bulayi ambapo ameeleza kuwa agizo la kusitisha matumizi ya taa hizo ni madai yasiyo na ukweli wowote hivyo wavuvi wa dagaa katika ziwa Victoria wanapaswa kupuuza na kuendelea na majukumu yao.

Kuhusu Athari za matumizi ya Taa hizo zinazotumia Betri za pikipiki, Bw. Bulayi amesema Tayari serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ilifanya Utafiti na kutoa mapendekezo ya aina ya Taa zinazokubalika katika Uvuvi ikiwamo za aina hiyo pamoja na zinazotumia mafuta ya Taa (Karabai) 

Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi nchini unazingatia sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015, Sheria ya Uvuvi na 22 ya mwaka 2003 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2009, na marekebisho ya mwaka 2018,2019,2020 na 2022 Huku Uvuvi wa Dagaa ukiwa chini ya kanuni ya 66 ya kanuni za mwaka 2009 na marekebisho yake kuhusu matumizi ya Taa za Sola.