
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa, amesema Serikali imeimarisha nguvu kazi katika Sekta ya Afya, kwakuongeza taasisi zinazotoa mafunzo ya Afya na upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa kada hiyo.
Waziri Mkuu Mhe.Majaliwa amesema hayo wakati akifungua rasmi Kongamano la majadiliano ya Kitaifa, kuhusu masuala ya rasilimali watu katika Sekta ya Afya, lililofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu, zinapatikana kwa kuendelea kutoa mikopo, kwa wanafunzi wenye sifa ikiwemo wanaosomea kozi za Afya ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100.
Katika kuendeleza rasilimali watu Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa, amesema suala hilo limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa kuongeza bajeti ya Sekta ya Elimu kila Mwaka, ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu wenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa.
Aidha, Mhe.Majaliwa amesema Serikali imeimarisha huduma za Afya ya msingi, huduma za Afya ngazi ya Wilaya na sasa inaimarisha huduma hizo kwenye ngazi za Halmashauri zote nchini, ili kupunguza umbali kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni.
"Kuhusu ajira na upangaji wa watumishi wa kada za Afya, katika kipindi cha Miaka Mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, watumishi Elfu 30,000 wameajiriwa wakiwemo Madaktari na kupangiwa vituo vya kazi vikiwemo vya vijijini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi." Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa