
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
"Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi," amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo katika kikao kilichofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.
Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza,pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.
"Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza, kwa kutathmini maombi 28 ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata. Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” amesema.
