
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Alexander Mnyeti, amesema serikali inaendelea kutekeleza mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa lengo la kuhakikisha afya za watoto zinaendelea kuimarika.
Mnyeti amesema kuwa watoto wengi nchini wakiwemo wa Mkoa wa Mwanza huondoka nyumbani asubuhi 3 kwenda shuleni bila kupata chakula chochote. Aidha, shuleni nako mara nyingi hawapati chakula na hivyo kuwafanya watoto kuwa na njaa, kukosa usikivu mzuri, na baadaye kutoona faida ya masomo.
Maziwa husababisha watoto kukua vizuri kimwili na kiakili hivyo yakitolewa kwa shuleni yataleta maendeleo mazuri kiakili na kimwili kwa watoto na siku za usoni tutakuwa na Taifa lenye watu wazuri walio na uelewa mkubwa. Ni muhimu kufanya hivi ili kuandaa Taifa lililo bora siku zote lakini kuwa na watoto wenye uelewa mkubwa.
Siku ya unywaji maziwa shuleni ni muhimu na ina lengo la kutoa hamasa ya kuboresha afya za watoto shuleni kupitia matumizi ya maziwa na bidhaa zake. Wataalamu wa lishe wanashauri kuwapa watoto mlo ulio bora zaidi na wenye kutoa virutubisho vyote muhimu na maziwa yamethibitika kuwa chakula muhimu zaidi kwa watoto na hata kwetu watu wazima.
Naibu Waziri Mnyeti ameyasema hayo, wakati akihitimisha Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza. Mnyeti amesema serikali imedhamiria kuhakikisha watoto wanakuwa na lishe bora hivyo ni lazima itekeleze mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa kuwa maziwa ni muhimu katika kuboresha afya za watoto.



Mnyeti amewasihi wadau wa Sekta Binafsi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha Watoto wanapata maziwa shuleni ili kuinua viwango vyao vya ufaulu. Inahitajika miundombinu na nguvu ya kusambaza maziwa shuleni hivyo ni vyema wadau wote kwa pamoja kujipanga kwa dhati kabisa ili kufanikisha jambo hilo. Aidha, wafugaji wametakiwa kuzalisha maziwa kwa wingi na wasindikaji na wadau wametakiwa kuhakikisha wanajisajili kwenye Bodi ya Maziwa Tanzania ili waweze kutambulika.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwekeza mazingira mazuri katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa nchi. Kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Tsh 1.02 Billion kwa ajili ya ununuzi wa Ng’ombe bora wa Maziwa 398 kwa wafugaji wadogo wa Maziwa kupitia AMCOS & VIkundi ya uzalishaji Maziwa ili kuongeza uzalishaji wa Maziwa hapa nchini. Pia serikali kupitia TADB Mradi wa TI3P imeweza kutoa ruzuku ya 25% ya gharama za Mitamba yenye thamani Tsh 257,256,625 ili kumpunguzia Mzigo wa Gharama za uendeshaji kwa mfugaji mdogo ili aweze kufuga kwa tija.
Mnyeti amewashukuru Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Serikali, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Gain Tanzania, Heifer International, ASAS Dairies LTD, Galaxy Food, Yoba for Life Foundation, wasindikaji wote wa kanda ya ziwa na wananchi kwa kuandaa, kushiriki na kufanikisha madhimisho hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. AminaMakilagi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema kwa upande wa mkoa walikuwa wakiendelea na utekelezaji wa mpango wa utoaji wa chakula shuleni hivyo kutokana na umuhimu wa maziwa latika kukuza lishe kwa Watoto watahakikisha suala la unywaji maziwa shuleni nalo linapewa kipaumbele ili kuhakikisha Watoto wanakuwa na afya bora.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TDB, Prof. Zacharia Masanyiwa amewasihi wazazi na walezi kuhakikisha Watoto wanapata lishe iliyo bora ambayo inapatikana kupitia matumizi ya maziwa. Aidha, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna wanavyoiwezesha Bodi ya Maziwa kutimiza majukumu yake katika kuwahudumia watanzania.
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Dkt. George Msalya amewasihi wafugaji kuhakikisha wanapeleka maziwa yao kwenye vituo vya kukusanyia maziwa ili yaweze kupimwa ubora wake kabla ya kwenda kwa walaji. Pia amewasihi wananchi kutumia maziwa ambayo yamesindikwa kwa kuwa ni salama.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Mpe Mtoto Maziwa kwa Maendeleo Bora Shuleni”, ikiwa na lengo la kuwa na Taifa lenye watoto wenye afya bora na uelewa wa juu sana na hivo kusaidia nchi kupata maendeleo zaidi. Wazazi na Walimu kwa pamoja tushirikiane kuwapa watoto maziwa yaliyosindikwa wawapo shuleni na nyumbani.
Pamoja na kuhitimisha maadhimisho hayo, Mnyeti pia amezindua Kituo cha Uhimilishaji Kanda ya Ziwa ambacho mtambo wake wa kuzalisha hewa baridi ya naitrojeni ulikuwa umeharibika toka mwaka 2016 lakini baada ya matengonezo yaliyofanyika mwaka 2023 sasa unafanya kazi vizuri.
Kituo hicho kunafanya kazi ya kuhifadhi na kusambaza mbegu bora za mifugo zinazozalishwa katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo mkoani Arusha. Kwa sasa kituo hicho kinatoa huduma ya uhimilishaji kwenye mikao ya Kanda ya Ziwa pamoja na mikoa jirani ya Katavi, Tabora na Kigoma. Kwa mwaka huu wa fedha hadi kufikia 26 Septemba 2023 jumla ya mirija 3,207 ya mbegu imesembazwa.
