Back to top

Serikali kufanyia marekebisho tozo, kanuni na sheria za uvuvi nchini.

14 December 2019
Share

Serikali imesema itaendelea kufanya marekebisho ya tozo, kanuni na sheria mbalimbali za uvuvi nchini ili wadau wa uvuvi waweze kufanya shughuli zao kwa tija zaidi na kuwataka maafisa uvuvi kuendelea kusimamia sheria zilizopo pamoja na wavuvi kutii sheria hizo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega amesema hayo Mkoani Mtwara wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kwa kujionea shughuli mbalimbali za uvuvi na kuzungumza na wavuvi katika baadhi ya vijiji vya Halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Mtwara ambapo amesema ziara yake imelenga kukusanya maoni kutoka kwa wadau hao.

Akizungumza na wadau wa uvuvi katika soko la samaki la Manispaa ya Mtwara, Mhe. Ulega amewataka maafisa uvuvi nchini kuwa na mahusiano mazuri na wavuvi pamoja na kuwasaidia wavuvi kutafsiri sheria mbalimbali ili wajiepushe na matumizi ya zana za uvuvi zisizotakiwa kisheria ambazo zinaweza kuwasababishia kutiwa hatiani kwa kukiuka sheria za nchi.

Aidha Mhe.Ulega amewataka maafisa uvuvi nchini kutojihusha na vitendo vya rushwa na kuwataka wavuvi wanaokutwa na hatia ya kujihusisha na kufanya shughuli zao kinyume na sheria ikiwemo uvuvi haramu kulipa faini wanayotozwa kwa kutumia utaratibu wa serikali uliowekwa.

Nao baadhi ya wavuvi wa soko la samaki la Manispaa ya Mtwara waliopata nafasi ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao kwa Naibu Waziri Ulega wameiomba serikali ya awamu ya tano kuwaboreshea zaidi mazingira ya kufanya shughuli zao kwa kuondoa kero mbalimbali wanazokabiliana nazo ili waweze kufanya shughuli zao ziwe na tija zaidi kwa kujiongezea mapato na kulipa kodi ya serikali. 

Wakati wa kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mtwara Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametembelea pia Kijiji cha Msanga Mkuu kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho wanaojihusha na shughuli za uvuvi na kuwataka kufanya kazi kwa kufuata sheria huku akiwataka pia maafisa uvuvi wakishirikiana na vyombo vya dola kutotumia nguvu kwa mtuhumiwa wa matumizi ya zana za uvuvi zisizotakiwa kisheria ambaye anatii sheria.