Back to top

Serikali kugharamia matibabu ya majeruhi 8 walioshambuliwa Msumbiji

18 July 2019
Share

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amesema serikali itagharamia matibabu ya majeruhi 8 walioshambuliwa kwa kupingwa risasi na wahalifu kwenye kijiji cha Mtole kata ya Palma nchini Msumbiji, na kulazwa hospital ya rufaa ya mkoa wa Mtwara ya Ligula.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo alipotembelea kijiji cha Kihamba kata ya Kitaya kuwapa pole wafiwa kufuatia tukio hilo lililoambatana na mauaji ya Watanzania kadhaa ambapo amewataka wananchi hao kushirikana na dola kuwafichua wahalifu wanaohatarisha amani kwenye mpaka huo.

Akitoa taarifa, mkuu wa wilaya ya Mtwara Evod Mmanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi wa wilaya hiyo amesema kwenye mashambulizi hayo wananchi 13 wamepoteza maisha, kati yao 11 ni Watanzania akiwemo aliyefariki hospital ya rufaa ya mkoa wa Mtwara akipatiwa matibabu na 2 raia wa Msumbiji. 

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota ambaye pia alitoa pole kwa wafiwa, ameiomba serikali kutazama upya katazo la kuwazuia wananchi wa kijiji hicho na vijiji vingine vinavyopakana na Msumbiji la kufuata mazao yao Msumbiji, kwa kutoa muda zaidi wa kuyafuata, ili wasiathirike kiuchumi.