Back to top

SERIKALI KUTAFUTA SULUHISHO MIALO KUFURIKA MAJI ZIWA TANGANYIKA

29 March 2024
Share

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutekeleza mkakati wa kutafuta suluhisho la kufurika kwa maji katika mialo ya ziwa Tanganyika mkoni Kigoma.

Akizungumza na wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi, Katibu mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, amesema serikali imeanza kufanya tathimini juu ya kufurika kwa maji kwa baadhi ya miundombinu ya mialo ya ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ambayo inatajwa kuchagizwa na mabadiliko ya Tabia nchi.

Prof. Shemdoe ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea baadhi ya mialo ikiwemo Kibirizi, Myobozi na Katonga ambayo baadhi ya miundombunu yake imefurika maji na kulazimu shughuli za biashara ya mazao ya uvuvi kusimama, na kusisitiza kuwa ofisi yake itashirikiana na  Sekretarieti za Mikoa ili kuona namna nzuri ya kurejesha huduma kwa wakazi ambao tegemeo lao ni ziwa Tanganyika

Prof. Shemdoe amesema maji hayo hayajaathiri tu masoko kwenye mialo bali hata chuo cha wakala wa elimu na mafunzo ya Uvuvi FETA kampasi ya Kigoma ambacho miundombinu yake imejaa maji na hivyo  kulazimika  kusitisha masomo kwa muda wa wiki mbili ili kutafutiwa eneo ambalo wataweza kuendelea na masomo yao huku serikali ikikamilisha mchakato wa kutafuta eneo zuri ambalo kampasi hiyo itajengwa upya.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara na wavuvi katika mialo  ya Kibirizi, Muyobozi na Katonga wamesema hali ya kujaa maji katika maeneo ya mialo ya ziwa Tanganyika imeathiri pakubwa shughuli zao kwani baadhi ya miundombinu iliyokuwa ikitumika kwa sasa imefurika maji.

Naye, mfanyabiashara wa mazao ya uvuvi, Bi. Anastazia Nicholaus alisema kupungua na kujaa maji katika Ziwa Tanganyika ni hali ambayo imekuwa ikijitokeza kwa kipindi cha masika japo kwa kipindi hiki maji yameanza kufurika zaidi ikilinganishwa na vipindi vya nyuma.