Back to top

SERIKALI KUWAPUNGUZIA MZIGO WAKULIMA WA KOROSHO

12 December 2025
Share

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Serikali itaendelea kuwapunguzia mzigo wakulima wa Korosho kwa kuwa na uhakika wa pembejeo za kilimo, na itahakikisha Korosho zote ghafi zinazosafirishwa zitumie Bandari ya Mtwara ili manufaa na maslahi yanayohusisha mchakato wa Korosho yanaacha neema katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Chongolo amebainisha haya wakati akitoa salamu za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye ziara ya kikazi mkoani humo, ambapo metoa maelekezo kwa Bodi ya Korosho Tanzania na kusisitiza Bodi hiyo kuendelea kulinda soko la awali la Korosho ili kukabiliana na walanguzi holela (maarufu kama kangomba). 

Waziri Chongolo ametembelea pia Kongani ya Viwanda iliyopo Maranje ambayo inalenga kuwa na viwanda vidogo vidogo vya kubangua Korosho, ili kuwezesha wakulima kupata tija na thamani zaidi kwenye zao hilo na kwamba kiwanda hicho kiwe na maabara ya kisasa kupima unyevu wa Korosho, ili kuhakikisha Korosho zinakuwa bora na shindanishi katika soko la Kimataifa hususani China na Vietnam.

Kadhalika Waziri Chongolo amekagua Kituo cha Tafiti za Kilimo cha TARI - Naliendele, na kuwataka watafiti wake kuongeza thamani za ubora wa mbegu na kupunguza visumbufu kwa kuhuisha teknolojia na sayansi katika zao la Korosho, akitolea mfano unyunywizaji wa dawa ya viuwadudu (Sulphur) kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki (drone). 

Aidha ameitaka TARI kutambua na kuthamini mchango wa watafiti wagunduzi wa mbegu bora ili wanufaike na kazi zao.