
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori, amewakemea baadhi ya Makandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea kuacha tabia hiyo huku akieleza kuwa Bodi haitasita kuwafutia usajili wa kampuni zao.
Amesema kwa sasa Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa miradi mingi kutekelezwa na Makandarasi wazawa lakini kuna baadhi wamekuwa wakitumia fursa hiyo kuijengea taswira mbaya tasnia hiyo kwa kufanya kazi bila kuzingatia weledi.
Mhandisi Rhoben Nkori amebainisha hayo Jijini Dar es Salaam, na kusema Makandarasi wasipotoa taarifa kwa wale watakaoonekana wanafanya kazi kwa mazoea basi watakuwa wanaunga mkono maovu hayo hivyo watakuwa wamejiweka katika mazingira magumu.





Ameeleza hayo Jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Makandarasi zaidi ya 170 waliokuwa wakishiriki mafunzo ya siku tatu yaliyokuwa yanalenga kuwajengea uwezo na ujuzi wa namna ya kuandaa zabuni, kujaza mikataba, utekelezaji wa mikataba ya ujenzi, elimu ya kodi na namna ya kuzisimamia na kuboresha kazi zao.
Amebainisha kuwa Serikali imejikita kutengeneza sera na mifumo rafiki ili Makandarasi wa ndani wafanye kazi kwa uhuru kwa kuzingatia weledi,sheria na taratibu zilizopo kama unaenda kukopa basi kopa kiasi kulingana na thamani ya mradi anaotekeleza.
Pia anasema Mkandarasi akifutiwa usajili hatakiwi kusajili Kampuni hiyo ndani ya muda wa miaka mitatu na mmiliki wa kampuni husika hawataruhusiwa kujiunga na kampuni nyingine ya ukandarasi hadi miaka miwili ipite.
Hata hivyo Wamiliki hawaruhusiwi kwenda kushika nafasi ya Mkurugenzi kwenye kampuni yeyote ile hadi kipindi cha miaka miwili ya kutumikia adhabu ya kufutwa iishe.
