
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imekubali kulipa Shilingi Bilioni 228 za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambazo ni deni la Wizara ya Mambo ya Ndani Shilingi Bilioni 45.4, Taasisi ya Mifupa (MOI) Shilingi Bilioni 18.2, NIDA Shilingi. bilioni 17.3 na Hospitali ya Benjamin Mkapa Shilingi Bilioni 129.
.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akijibu hoja za ripoti ya CAG ya 2021/2022, kuhusu hoja ya serikali kutokulipa madeni ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambapo amebainisha kuwa madeni hayo yatalipwa ili kulinda uhai na uendelevu wa Mfuko.
.
"Kila senti inayotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenda kwenye Sekta ya Afya tutaisimamia, na nitume salamu kwa Watendaji wote wa MSD na wengine wa Sekta ya Afya watakaofanya ubadhirifu hatutawavumilia, tutachukua hatua mara moja ili kulinda fedha za Serikali" amesema Waziri Ummy.
.
Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka historia ya kutoa fedha Tsh. Trilioni 6.7 kwenye Sekta ya Afya jambo ambalo halijawahi kutokea huku akimpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Bw. Charles Kichele kwa kufanya kazi vizuri ya kikatiba ya kudhibiti na kukagua fedha za Watanzania.
