
Wanawake katika halmashauri ya Wilaya ya Tandaimba mkoani Mtwara wameiomba serikali kukomesha tabia ya udhalilishaji dhidi ya wanawake hasa kipindi hiki ambapo baadhi ya vyama vya siasa vinaelekea katika chaguzi za ndani ili kutoa fursa ya kushika nafasi mbalimbali za maamuzi ndani ya vyama hivyo lakini pia nje ya vyama.
Kauli hiyo ya wanawake wameitoa katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ambayo Kiwilaya imefanyika katika Kata ya Mkwiti kijiji cha Liko kombe wilaya ya Tandaimba mkoani Mtwara.
Baadhi ya wanawake wamesema licha ya kupambana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vya siasa na nje ya siasa wamekuwa wakipata wakati mgumu hasa kudhalilishwa na jinsia ya kiume.
Wamesema tabia hiyo haina budi kukomeshwa kwani imekuwa silaha kubwa kwa baadhi ya wanaume kuwachafua wanawake wanaogombea pamoja nafasi mbalimbalimbali za maamuzi hasa za ubunge na udiwani.
Wamesema wanaweake wengi wamenyimwa haki ya msingi ya kushika nafasi hizo za maamuzi na baadhi yao kupoteza ujasiri wa kuendelea kupambania nafasi hizo na kutaka ifike mwisho na sheria itumike ipasavyo kukomesha tabia hiyo.
