Back to top

Serikali yaombwa kutoa mafunzo ya lugha ya alama katika sekta ya afya.

21 May 2018
Share

Watu wenye matatizo ya kusikia nchini (VIZIWI) wameiomba serikali kutoa mafunzo ya kutafsiri lugha ya alama kwa watoa huduma za kijamii ikiwemo katika sekta ya afya na elimu ili kuwapunguzia changamoto mbalimbali zinazowakabili za kushindwa kuelewana wakati wa huduma hatua ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa anapofika hospitali.

Mwenyekiti wa Chama cha walemavu nchini Nitrose Mlawa akizungumza jijini Tanga amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa kanuni za kimataifa za huduma za walemavu ambapo Tanzania imeingia mkataba wa utekelezaji wa huduma kwa walemavu mwaka 2010 lakini hadi sasa  walemavu hao wamekuwa wakipata shida ya kukosa wakalima hasa maeneo yanayotoa huduma za afya.
  
Awali akifafanua katika Mkutano wa kitaifa wa kuwasilisha taarifa ya utafiti uliofanya na wanasheria katika masuala ya uwajibikaji wa jamii na mchango wa serikali za mitaa,mratibu wa kitaifa wa mkutano huo Lupi Maswanya amesema utafiti huo umeonesha kuwa ingawa serikali imeingia mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu na kutengeneza sheria,lakini bado utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na kuweka wakalimani katika maeneo muhimu bado ni changamoto.

Kufuatia hatua hiyo Makamu mkuu wa shule ya sekondari ufundi Tanga Adamu Mkumulwa amesema baadhi ya wanafunzi walemavu wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa wakalimani katika shule hiyo kongwe ya kwanza ya sekondari kuanzishwa nchini ambapo wanachanganywa na wanafunzi wa kawaida na kushindwa kuelewa mwalimu anachofundishwa.