Back to top

SERIKALI YASITISHA UTOAJI WA LESENI, VYETI NA VIBALI VYA MKONO

12 July 2022
Share

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) imesitisha rasmi utaratibu wa uandaaji na utoaji wa vibali, vyeti na leseni zinazoandikwa kwa mkono au maombi ya kumbukumbu za malipo (control number) kwa njia ya simu kwa ajili ya biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi kuanzia  tarehe 12.07.2022.

Hayo yamesemwa leo (12.07.2022) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Bw.Tixon Nzunda kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo imetokana na kuanza kwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa utoaji na usajili wa vibali, leseni na vyeti unaojulikana kama “Mifugo Integrated Management Information System (MIMIS)” ambao unapatikana kupitia kiunganishi (link) cha https://mimis.mifugo.go.tz.

“Lengo la mfumo huu ni kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara za mifugo na mazao yake na kuwawezesha wafanyabiashara wa maziwa, nyama, vyakula vya wanyama, ngozi na wadau wengine wa sekta ya Mifugo kupata vibali au kufanya usajili wa biashara za mifugo na mazao yake popote walipo na kwa wakati bila kulazimika kufika kwenye ofisi za Wizara” Amesisitiza Nzunda

Nzunda ameongeza kuwa mbali na wafanyabiashara, mfumo huo pia utawawezesha wataalam wa afya ya mifugo kujisajili na kuhuisha taarifa zao popote walipo hatua itakayowafanya kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Kwa wale wafanyabiashara, wataalam na wadau ambao leseni au vyeti vyao havijamaliza muda wake wa matumizi, wanatakiwa kujisajili kwa kuingiza taarifa za sasa za usajili wa biashara pamoja na leseni au cheti husika bila gharama yoyote” Alimalizia Nzunda.

Kuanza kutumika kwa mfumo huo ni miongoni mwa hatua za uboreshaji wa huduma kwa wadau wa sekta ya Mifugo ili kuwarahisishia kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuongeza kipato na  kutokana na shughuli hizo.