Back to top

Serikali yatakiwa kuongeza kasi udhibiti wa vitendo ujangili.

12 May 2018
Share

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka mikoa ya Manyara, Katavi, Mara na Simiyu wameitaka serikali kuongeza kasi ya udhibiti wa vitendo haramu vya ujangili vinavyofanywa katika hifadhi za taifa nchini hali itakayosaidia kulinda sekta ya utalii inayochangia zaidi ya asilimia ishirini ya fedha za kigeni zinazoingia nchini.

Wakizungumza na ITV wakati wa zoezi la ugawaji wa magari yanayopelekwa katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya ujangili yaliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii baadhi ya wabunge wamesema licha ya jitihada zinazofanywa na serikali bado kuna haja ya kuongezwa nguvu ya kupambana na vitendo haramu vya ujangili kwa kutoa elimu kwa wananchi.

Haya ni baadhi ya magari yanayopelekwa katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya ujangili ambayo yametolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii 

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangala.amesema serikali imeamua kutoa magari hayo ili kuongeza kasi ya udhibiti wa vitendo haramu vya ujangili katika baadhi ya maeneo nchini ambapo amesema hali ya vitendo vya ujangili nchini vimepungua kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangala akiwa akijadiliana jambo na baadhi ya wabunge kutoka mikoa ya Manyara, Katavi, Mara na Simiyu ambao wameitaka serikali kuongeza kasi ya udhibiti wa vitendo haramu vya ujangili.