Back to top

SERIKALI YAWATANGAZIA VITA WAVUVI HARAMU

17 May 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali sasa itaweka nguvu kubwa kukomesha uvuvi haramu katika ziwa Victoria baada ya hatua kadhaa zilizochukuliwa hapo awali ikiwemo kuwashirikisha wavuvi wa kanda ya ziwa kutokuzaa matunda.

Mhe.Ndaki ametoa kauli hiyo alipokuwa akiongea na wadau wa sekta ya uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ziwa Victoria kilichofanyika Mkoani Mwanza.

Amesema mwaka jana serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya uvuvi waliandaa mpango shirikishi ambao ulianisha kila mdau na jukumu lake katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa Victoria lakini matokeo yake wadau hao hawakujali na sasa uvuvi haramu umeongezeka maradufu.

"Uvuvi haramu sasa hivi ni mkubwa kwenye ukanda wetu wa ziwa Victoria na sisi wizara tumepewa jukumu la kusimamia rasilimali hizi, Mhe.Rais atatushangaa sana kuona wizara iliyopewa dhamana ya kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa, hazilindwi, sasa wakati tunatafuta mbinu endelevu ya kulinda rasilimali hizi, kuanzia sasa kwenda mbele tutatumia nguvu kuzuia uvuvi haramu"Amesema Ndaki.

Ameongeza kuwa serikali haitavumilia watu wachache wenye kutaka kujinufaisha wao binafsi huku akiongeza kuwa watawashughulikia wale wote wanaojihusisha na uvuvi haramu kuanzia wavuvi, wasambazaji wa nyavu zisizo halali, na watakamata vyombo vyote vitakavyotumika kubebea au kuhifadhi mazao yaliyovuliwa kwa njia ya haramu katika mikoa yote inayozunguka ukanda wa ziwa Victoria.

Aidha, Waziri Ndaki amewaeleza wadau wa uvuvi katika kikao hicho kuwa serikali imepokea changamoto zao na watazifanyika kazi lakini nguvu kubwa kwa sasa itawekwa katika kupambana na uvuvi haramu kwa sababu kama rasilimali za uvuvi zikitoweka hizo changamoto nyingine kama za tozo na utafutaji wa masoko hazitakuwa na maana yoyote.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia sekta ya uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa serikali imesikiliza kilio cha wavuvi kuhusu tozo na imezishughulikia kwa kiasi kikubwa na hivi karibuni michakato ikikamilika serikali itatoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa na nafuu kubwa kwa wavuvi.

Changamoto kubwa zilizowasilishwa na wadau wa sekta ya uvuvi kwa serikali ni pamoja na uvuvi haramu, matumizi yasiyosahihi ya taa za kuvulia samaki, mlundikano wa tozo kwa mazao ya uvuvi na uhaba wa masoko ya mazao ya uvuvi.

Wadau walioshiriki kikao hicho ni pamoja na viongozi kutoka serikalini, wawakilishi kutoka katika Benki, wavuvi wa Dagaa, wavuvi wa Sangara, wachakataji wa mazao ya uvuvi, wawakilishi wa vyama vya ushirika,wazalishaji wa zana za uvuvi, wafanyabiashara wa taa za sola, wafanyabiashara wa mabondo na wafugaji wa samaki kwenye vizimba.