Back to top

Shehena ya Bangi yanaswa Arusha ikisafirishwa nchi jirani.

14 July 2020
Share

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limekamata shehena ya Bangi inayokadiriwa kufikia magunia 15 yakisafirishwa kwenda nchi jirani kwa kutumia gari dogo la abiria aina ya Noah.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha ACP Salumu Hamduni amesema bangi hiyo imekamatwa katika Kijiji cha Albomba wilaya ya Longido baada ya polisi kulitia shaka gari hilo na kuanza kulifuatilia.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni wakati polisi wanafukuza gari hilo linalofanya safari zake kati ya Arusha na Namanga lenye namba za usajili T302BXZ ilipata pancha na dereva akalitelekeza akakimbia japo alikamatwa baada ya saa sita kufuatia msako mkali ulioendeshwa na Jeshi la Polisi.

Aidha kamanda Hamduni amewapongeza na kuwashukuru askari waliofanikisha kukamata bangi hiyo na kwamba taratibu za kuwapa zawadi kama  motisha wa kuonyesha uadilifu na utendaji kazi mzuri na uliotukuka.

"Askari wote wanafanyakazi nzuri lakini wapo wanaojituma zaidi ,hawa utaratibu wa kuwapa motisha uko wazi na utafuata ,na kumbuka kuwa zawadi za motisha ziko nyingi sio lazima fedha"alisema Kamanda Hamduni.

Kamanda Hamduni pia amewapongeza viongozi wa wilaya ya Longido kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa kwa jeshi la polisi katika kukabiliana na uhalifu .

"Haya ni moja ya matunda ya ushirikiano wa watendaji wa Halmashauri ya wilaya hii na vyombo vya dola,na huu ni mfano unaotakiwa kuigwa na wilaya zingine"alisema Kamanda Hamduni.

Awali mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe amesema pia mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano unaotolewa na wananchi wakiwemo walinaoishi maeneo ya mpakani.

"Kwa muda mrefu sasa tumekuwa na kazi kubwa ya kuwaelimisha wananchi wa vijiji vya mpakani na nchi jirani juu ya umuhimu wa kutoa ushirikiano ukiwemo wa taarifa za wahalifu na kwa sasa asilimia kubwa wanatoa taarifa"alisema Mwaisumbe Dc Longido .

Shehena hiyo ya Bangi imekamatwa ikiwa ni siku chache baada ya bangi nyingine kukamatwa katika wilaya ya Arumeru tukio ambalo lilipelekea baadhi ya watendaji kuwajibishwa.

Kwa mujibu sheria gari ama chombo cha moto kitakachokamatwa na dawa za kulevya kinataifa jambo linaloonyesha kuwa basi hilo dogo kwa sasa kitataifishwa .

Licha ya kuwepo kwa matukio kadhaa ya matumizi ya magari ya abiria kusafirisha madawa ya kulevya ,tukio hili la kutumia  basi dogo aina ya Noah ni la Kwanza katika wilaya ya Longido na pia mkoa wa Arusha.