Back to top

Shule kufunguliwa Juni 29, shughuli za harusi na mambo mengine ruksa.

16 June 2020
Share

Rais Dkt.John Pombe Magufuli ametangaza kufunguliwa kwa shule zote zilizofungwa kwa tahadhari ya maambukizi ya virusi vya Corona, zifunguliwe kuanzia Jumatatu tarehe 29 Juni 2020.

Akilihutubia na kulivunja bunge la kumi na moja jijini Dodoma, Rais Magufuli amesema amechukua uamuzi kutokana na kupungua kwa kiwango cha janga la Corona.

Aidha, ameruhusu shughuli nyingine zilizosimaishwa ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo kama vile ndoa na harusi.

Hata hivyo, amewataka wananchi waendelee kuchukua hadhari dhidi ya virusi hivyo zinazotolewa na wataalam wa afya na viongozi wa serikali, na kusisitiza kuwa virusi hivyo vipo.

Kuhusu utendaji wa serikali, amesema bajeti ya maendeleo katika miaka mitano iliyopita imeongezeka kutoka asilimia ishirini na sita hadi asilimia arobaini.

Amesema katika kipindi hicho, ukusanyaji wa mapato uliongezeka kutoka shilingi bilioji mia nane hamsini hadi shilingi trilioni moja nukta tatu kwa mwezi.

Rais amesema katika kipindi hicho, serikali ilichukua hatua mbalimbali zilizolenga kuimarisha uchumi na kuliwezesha taifa kuimarisha huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu, mawasiliano.

Amewashukuru viongozi wa serikali za awamu zilizotangulia, waliopo, wabunge na wananchi kwa ushirikiano wao ulioiwezesha serikali kupata mafanikio hayo.