
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa, amewataka Wakurugenzi wa Halmasahauri nchini, kuhakikisha maeneo yote ya huduma za jamii yanapimwa kwa lengo la kulinda maeneo hayo.
Waziri Silaa amesema hayo wakati akizungumza na uongozi pamoja na watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Tabora akiwa kwenye ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri Kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Amesema, kwa sasa ndani ya wizara yake kuna mabadiliko wanayokwenda kuyafanya katika maeneo yanayoonekana kama kikwazi kwa sekta hiyo na kutolea mfano wamiliki wa ardhi kuogopa kuchukua hati kwa hofi ya kulipa kodi ya ardhi sambamba na uwezo wa kifedha baadhi ya halmashauri katika kutekeleza majukumu ya sekta ya ardhi.

Aidha, ameweka wazi kuhusu suala la usimamizi wa sheria za ardhi ambapo amesema halmashauri zimekuwa na msukumo mkubwa kutoka kwa wananchi kuhusu suala hilo ambapo amesema hakuna msukumo unaopelekea uvunjifu wa amani na kusisitiza kuwa maeneo ya wazi yabaki wazi na yale ya huduma kama taasisi yabaki kuwa ya taasisi.
Aidha, katika ziara hiyo waziri Silaa amehimiza pia suala la usimamizi wa sheria katika kutekeleza majukumu sambamba na kuziagiza mamlaka za uhifadhi nchini kuhakikisha zinaongeza nguvu katika kulinda maeneo ya hifadhi ili wananchi wasiweze kuvamia maeneo hayo.
Waziri Silaa amehitimisha ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Tabora ambapo mbali na kuzungumza na watumishi alipata fursa ya kutembelea ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora, Chuo cha Ardhi Tabora pamoja na kitega uchumi cha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
