Back to top

SILAA AHIMIZA MA-RC KUTEKELEZA MAAMUZI BARAZA LA MAWAZIRI VIJIJI 975

14 September 2023
Share


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amehimiza wakuu wa mikoa nchini, kuhakikisha wanatekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

Waziri Silaa akiwa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, amesema  atahakikisha serikali inapotoa kauli lazima itekelezeke kwa kuwa ndiyo kazi aliyotumwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan na kuweka bayana kuwa, kazi aliyotumwa ataifanya mapema na kupeleka majibu ya mpango wa serikali kwa wananchi wa Nanyumbu ili kupunguza taharuki.

Waziri Silaa amesema hayo wakati akizungumza na uongozi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, akiwa kwenye ziara ya siku moja kufuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumzi ya adhi katika vijiji 975.

Alisema, ameridhishwa sana na tekelezaji wa maamuzi hayo kwa mkoa wa Mtwara kupitia wilaya ya Nanyumbu ambapo kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi wilaya hiyo imeweza kutekeleza maagizo hayo kwa asiliamia mia moja.

Aidha, alibainisha kuwa, migogoro ya ardhi inahusisha watu na pale utatuzi wake unapocheleweshwa unaleta mgogoro mwingine mkubwa kuliko wa awali jambo alilolieleza utatuzi wake unaweza kuwa mgumu kwa sababu utatuzi wa pili unaondoa imani ya wananchi kwa jambo lililoamuliwa na serikali kuwa linaweza kutekelezeka kwa haraka.

Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 yanafuatia timu iliyoundwa kuchunguza changamoto za uvamizi wa maeneo ya hifadhi ambapo timu hiyo iliwasilisha taarifa ya migogoro katika vijiji 366 na ndipo ikaundwa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta mwaka 2019 iliyokuja na mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 huku vijiji 55 utatuzi wake ukisalia.

Wizara za kisekta zinazohusika katika utatuzi huo ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama mwenyekiti, Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Maji, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), TAMISEMI na Wizara ya Ulinzi.