SIMBA MAARUFU 'BOB JUNIOR' AUAWA

Simba maarufu Kaskazini mwa Tanzania aliyeishi katika Hifadhi ya Serengeti, ‘Bob Junior’ ameuawa baada ya kushambuliwa na kundi la Simba watatu waliokuwa na lengo la muda mrefu la kuuangusha utawala wake, Mamlaka za hifadhi nchini Tanzania zimethibitisha kifo hicho kilichotokea Jumamosi iliyopita.

Simba hao watatu waliowahi kujaribu kujisimika ufalme walilelewa na ‘Bob Junior’ tangu wakiwa wadogo lakini majaribio ya kufanya mapinduzi mara kadhaa ili kuuangusha utawala wa Bob Junior haukufanikiwa na badala yake walikimbizwa katika maeneo hayo, yaliyopo mashariki mwa hifadhi hiyo.

Simba ‘Bob Junior’ akisaidiana na kaka yake, Joel walitawala kwa zaidi ya miaka mitano na kuwa miongoni mwa Simba waliotawala kwa kipindi kirefu zaidi kabla ya kufanyika mapinduzi.

Mwandamizi wa hifadhi hiyo, Fredy Shirima amesema tukio hilo ni asilia katika hifadhi lakini pia hutokea zaidi kwa Simba ambao hushikilia ngome dhidi ya wengine wanaoitaka ngome.

Shirima anasema, "Bob Junior aliuawa siku ya Machi 11, akishambuliwa na Simba watatu ambao walikuwa sehemu ya kundi la simba saba waliokuwa wanapanga mapinduzi.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo,Bob Junior ni simba aliyejibebea sifa kwa kuwa mpole na anayekuwa na utulivu anapoona watalii.

Shirima anasema, ‘Bob Junior’ pia alikuwa na sifa za kipekee kama vile kuwa na manyoya mengi zaidi kuliko simba wengine lakini mwenye kuvutia kwa muonekano na hutulia pale anapopigwa picha.

Wadau wa utalii wamesikitishwa na kifo cha simba huyo, huku ikimtaja kuwa ndiyo simba bora na mtulivu kuwahi kuonekana katika hifadhi ya Serengeti.