Back to top

"Sote tumeshuhudia Simba wakiendelea kuupiga mwingi".Majaliwa.

06 April 2022
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza timu ya mpira wa miguu ya Simba kwa kuipeperusha vema bendera ya Taifa katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika.

“Mwenye macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa. Hakika kwa mpira mzuri wanaocheza wanakonga nyoyo ya mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.”

Ametoa pongezi hizo leo (Jumatano, Aprili 6, 2022) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.

 
Pia, Waziri Mkuu amewapongeza wachezaji mahiri wa vilabu mbalimbali vya mpira wa miguu nchini vikiwemo Yanga 9Timu ya Wananchi), Simba (Wekundu wa Msimbazi) Namungo (Wauaji wa Kusini) Azam (Wazee wa Lambalamba), Vilabu vingine ni Biashara United - Wanajeshi wa Mpakani; Dodoma Jiji - Walima Zabibu; Tanzania Prison – Wajelajela; Mtibwa Sugar - Wakata Miwa na Kagera Sugar – Wanankurukumbi; KMKM, Mlandege, Malindi, Mafunzo na vilabu vinginevyo.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapiga hatua.

Amesema lengo ni kuimarisha michezo, sanaa na utamaduni ili ziweze kuchangia vema katika Pato la Taifa sambamba na kuzalisha ajira kwa vijana, kutangaza utalii, kuimarisha umoja wa kitaifa na afya za Watanzania.
 

Kwa upande wa mchezo wa ngumi, Waziri Mkuu amewapongeza wanamasumbwi Hassan Mwakinyo, Tonny Rashid, Twaha Kiduku na Ibrahim Class kwa ushindi mnono uliowawezesha kupata mikanda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa waliyoshiriki.