
Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Ndugai amefariki dunia leo Jumatano, Agosti 6, 2025 jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson.
"Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma. Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu," amesema Mheshimiwa Spika.
Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya Marehemu inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.