Back to top

TABORA KUWA KINARA PROGRAMU YA BBT MIFUGO NCHINI - ULEGA

01 June 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema kufuatia Mkoa wa Tabora kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo hapa nchini, wamepanga kuanzisha programu kabambe ya BBT Mifugo itakayowawezesha vijana kunenepesha mifugo na kuufanya mkoa huo kuwa kinara na lango kuu la kuuza nyama bora ndani na nje ya nchi.

Amesema Tabora ni mkoa uliobarikiwa kuwa na eneo kubwa la ardhi na rasilimali nyingi ya mifugo hivyo anaona mkoa huo una kila sababu ya kuwa kinara wa kufanya biashara ya mifugo.

Waziri Ulega ameeleza hayo katika mkutano wa hadhara aliyoufanya Wilayani Kaliua mkoani.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, tunataka kuufanya mkoa wa Tabora kuwa ndio lango la kuvunia mifugo, vijana wawekeze kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa mifugo na mazao yake ili waweze kuuza nyama  ndani na nje ya nchi, na wakiweza kufanya hivyo watakuza kipato chao na Taifa kwa ujumla" Amesema Ulega

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, sisi tupo tayari kuanzisha programu ya BBT hapa Tabora  kwa sababu rasilimali ipo ya kutosha hivyo ni rahisi kupata matokeo kwa haraka, muhimu ni kuifungamanisha rasilimali hiyo katika mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji mpaka katika masoko" Amefafanua

Amesema kwa kuwa programu hiyo walishaianzisha katika Mikoa ya Mwanza, Kagera na Tanga hivyo ni rahisi kuanzisha pia mkoani Tabora, na mipango ni kuifanya BBT Mifugo ya Tabora kuwa ya kwanza katika ufugaji bora na uuzaji wa nyama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi. Dkt.Batilda Burian amemshukuru Waziri Ulega kwa mipango hiyo, huku akimuhakikishia kuwa tayari wana eneo la 
hekari 6000 lililopo Wilayani Kaliua  ambalo watalitumia kwa ajili ya programu hiyo ya BBT Mifugo. 

Aidha, amesema kuna hekari nyingine 40,000 ambazo zipo Wilayani  Nzega ambazo watazitumia pia kufanya ufugaji wa kisasa ikiwemo kulima malisho kwa ajili ya mifugo yao na kuuza ndani na nje ya nchi.